UGONJWA WA UTI WA MGONGO( MENINGITIS)

Chat with female and males
Ugonjwa wa uti wa mgongo hutokea iwapo utando unaofunika ubongo na uti wa mgongo utapatwa na maambukizi.

Ugonjwa wa Uti wa mgongo husababishwa na nini?
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea mbalimbali vya makundi ya bakteria, virus na hata fungus. Tukivigawanya visababishi hivi katika makundi haya, tutaona kuwa bakteria wanaosababisha ugonjwa wa uti wa mgongo ni kama vile; bakteria wajulikanao kama Beta-streptococci, Hemophilus influenza, Escherichia coli, Listeria monocytogenes, Neisseria meningitides, Streptococci pneumoniae pamoja na Mycobacteria tuberculosis, ambao pia ni maarufu kwa kusababisha ugonjwa wa kifua kikuu.

Aidha kutoka kundi la virus, virus wanaojulikana kwa kusababisha ugonjwa huu wa uti wa mgongo ni pamoja na Herpes simplex type 2, HIV pamoja na Varicella zoster.

Vimelea vya fungus ambavyo hujulikana kwa kusababisha ugonjwa wa uti wa mgongo ni pamoja na wale wajulikanao kama Coccoidiodomycosis pamoja na Cryptococci meningetides.



Dalili na viashiria vya uti wa mgongo ni pamoja na

- Shingo kukakamaa na kuwa ngumu isivyo kawaida
- Mgonjwa kujihisi homa kali
- Maumivu makali ya kichwa
- Mgonjwa kupoteza fahamu
- Mgonjwa kupatwa na degedege (seizures) na mwili kukakamaa
- Mgonjwa kushindwa kuvumilia mwanga (photophobia)
- Mgonjwa kutoweza kukaa sehemu yenye makelele (phonophobia)
- Kwa watoto, kuvimba utosi
Aidha, wakati wa kumfanyia mgonjwa uchunguzi, daktari anaweza kuangalia pia viashiria vingine vinavyoonesha kuwepo kwa ugonjwa wa uti wa mgongo. Ishara hizi ni kama vile

Mgonjwa uhisi maumivu kwenye uti wa mgongo yanayozuia kukunjua goti wakati anapofanyiwa uchunguzi wa kukunjua goti lake (pain limits passive extension of the knee). Ishara hii huitwa ishara ya Kerning au Kerning's sign.
Wakati mwingine mgonjwa anapoelekezwa kujitahidi kukunja shingo, miguu (yaani paja pamoja na goti) navyo hujikunja pia (flexion of the neck causes involuntary flexion of the knee and hip). Ishara hii huitwa ishara ya Brudzinski au Brudzinski’s sign.
Vipimo na uchunguzi

Pamoja na kumchunguza mgonjwa kuhusu kuwepo kwa dalili na viashiria vya ugonjwa huu wa Uti wa mgongo, daktari pia anaweza kufanya vipimo vifuatavyo;

- Kuchunguza damu ya mgonjwa kwa ajili ya kuangalia uwepo wa vimelea vinavyosababisha ugonjwa na pia kufahamu ni aina gani ya vimelea hao. Hali kadhalika, damu inaweza pia kutumika kuotesha vimelea maabara ili kugundua aina ya vimelea na dawa gani nzuri zinazofaa kwa ajili ya matibabu (culture and sensitivity).
- Kipimo kinachofanyika kwa kuchukua maji ya uti wa mgongo wa mgonjwa na kuyachunguza maabara ili kutambua uwepo wa vimelea, aina ya vimelea na dawa zinazofaa kutibu vimelea hao (Lumbar puncture).
- Kwa baadhi ya maeneo yenye vifaa kama CT-scan na MRI, mgonjwa pia huweza kuchunguzwa kwa kutumia vifaa hivi ili kufahamu uwepo wa ugonjwa, sehemu lilipo na madhara yaliyosababishwa na ugonjwa huu wa uti wa mgongo. Hata hivyo vipimo hivi haviwezi kutambua aina wala dawa ya kutibu vimelea vinavyosababisha ugonjwa huo.

Matibabu ya ugonjwa wa Uti wa Mgongo
Kwa wagonjwa waliopoteza fahamu ni vizuri kuhakikisha wanapumua vizuri, na njia za hewa ziko wazi. Halikadhalika, iwapo itathibitika kuwa bakteria ndiyo wanaosababisha ugonjwa huu, mgonjwa anaweza kupewa mojawapo ya dawa hizi za antibiotiki kama cefotaxime au Cefriaxone. Aidha baadhi ya madaktari hupendelea kuongeza dawa za steroids kama dexamethasone kama sehemu ya matibabu.

Iwapo itathibitika ugonjwa huu umesababishwa na virus, dawa kama Acyclovir huweza kutumika. Hali kadhalika, ikithibitika kuwa vimelea waliosababisha ugonjwa huu ni wa kundi la fungus, dawa kama Amphotericin B au flucytosine zaweza kutumika. Mgonjwa pia hupewa Paracetamol kwa ajili ya kushusha homa na kuondoa maumivu ya kichwa.



Ugonjwa wa uti wa mgongo unaweza kusababisha

- Kuamshwa kwa chembechembe za damu zinazo sababisha damu kuganda kitaalamu – Disseminated Intravascular Coagulopathy (DIC).
- Kuvuja damu kwa katika tezi za adrenalin na kupelekea kutokea kwa ugonjwa ambao kitaalamu unaitwa – waterhouse friderichsen syndrome.
- Kwa watoto, ugonjwa huu unaweza kusababisha mtoto kuwa na kichwa kikubwa - hydrocephalus.

Post a Comment

0 Comments